Jumatano, 29 Juni 2016

       MAAMBUKIZI KATIKA NJIA YA MKOJO (U.T.I)
Maambukizi katika njia ya mkojo ni ugonjwa au maambukizi yanayotokea kwenye njia ya mkojo na kusababisha maumivu, homa, kukosa nguvu, harufu mbaya ya mkojo na maumivu wakati wa kukojoa. Husababishwa na bakteria ambao wanaingia kwenye mwili kupitia kwenye uke au uume wakati wa kujamiiana, kuwekewa mpira wa kukojolea, wakati wa kutawadha au ukuaji wa bakteria wakati wa uvaaji pedi na nguo za ndani.
Maambukizi haya huweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kupitia kujamiiana, na pia mtu anaweza kuyapata bila hata kujamiiana kama ilivyooneshwa hapo juu.
Huweza kumpata mtu yeyote, lakini watu walio katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi haya ni wanawake, na zaidi ni wanawake wajawazito. Pia wazee, wagonjwa wa tezi dume, wagonjwa waliowekewa mipira ya kukojolea, wagonjwa wa kisukari na wagonjwa wenye upungufu wa kinga ya mwili.
JINSI MAAMBUKIZI YA NJIA YA MKOJO (U.T.I.) YANAVYOTOKEA NA KUENEZWA
Maambukizi ya njia ya mkojo huwapata watu kupitia njia zifuatazo
- Kujamiiana na mtu mwenye maambukizi bila kutumia kinga
- Kueneza bakteria kutoka kwenye kinyesi (njia ya haja kubwa) kwenda kwenye uke (njia ya mkojo) wakati wa kujitawadha kwa kunawa kutokea nyuma (kwenye njia ya haja kubwa) kuja mbele (kwenye njia ya haja ndogo)
- Kukua kwa bakteria kupitia mipira ya kukojolea wagonjwa, pedi na nguo za ndani
- Kutawadha maji yenye bakteria wanaoweza kusababisha maambukizi katika njia ya mkojo
- Kukua kwa bakteria kupita kiasi katika njia ya mkojo kutokana na kupungua kwa kinga ya mwili
DALILI ZA MAAMBUKIZI KATIKA NJIA YA MKOJO (UTI) Maambukizi katika njia ya mkojo huwa na dalili zifuatazo
- Maumivu wakati wa kukojoa na kuhisi kama unaungua kwa ndani ya njia ya mkojo
- Kujisikia kukojoa mara kwa mara, ila kupata mkojo kidogo tu
- Maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo
- Homa
- Uchovu na kupungukiwa na nguvu
- Rangi ya mkojo kubadilika na kuwa kama nyekundu au pinki (japo kwa mbali)
- Mkojo kuwa na uchafu kama 
- Kichefuchefu na kutapika

MADHARA YA BAADAE YA MAAMBUKIZI KATIKA NJIA YA MKOJO (U.T.I)Mara nyingi ugonjwa huu hudhibitiwa vizuri na dawa na hakuna madhara makubwa yatakayojitokeza. Vinginevyo kama ukichelewa kutibiwa unaweza kupata uharibifu wa Ini. Matokeo yake ni kujifungua kabla ya miezi tisa na kuzaa watoto wenye uzito mdogo. Ni vyema kupata matibabu mazuri na kwa wakati ili kuweza kuzuia uharibifu na matatizo mengine yoyote yanayoweza kujitokeza baadae.
MATIBABU YAKE
Kuna dawa nyingi sana za kutibu ugonjwa huu wa maambukizi katika njia ya mkojo. Cha msingi ni kufanya vipimo na kujua bakteria au wadudu wengine waliosababisha ugonjwa na kujua dawa nzuri zaidi kwa ajili ya kuwaua. Unashauriwa kumuona daktari na kupata matibabu sahihi ili kuweza kupona kabisa ugonjwa huu.
Zipo dawa nyingi kwa ajili ya ugonjwa huu. Baadhi yao huweza kutumika kwa mtu yeyote (Mifano Amoxicillin na Ampicillin) na nyingine haziwezi kutumika kwa baadhi ya watu kama vile Doxycycline haiwezi kutumika kwa watoto na Tetracycline haiwezi kutumika kwa akina mama wajawazito.


Usitumie dawa yoyote bila kushauriwa na daktari. Na hakikisha unatumia dawa zote kama ulivyoelekezwa na daktari na mfamasia, ikiwa ni pamoja na kumaliza dozi hata kama utajihisi umepona kabla ya kumaliza dawa.












JINSI YA KUJIKINGA DHIDI YA MAAMBUKIZI YA NJIA YA MKOJO (U.T.I.)Uzuri wa maambukizi haya ni kwamba huweza kuepukwa au kuzuiliwa kabisa. Mtu anaweza kujikinga kwa
- Kuepuka kujamiiana bila kutumia kinga
- Kunawa vizuri wakati wa kujitawadha kwa kuanzia mbele (njia ya haja ndogo) kwenda nyuma (njia ya haja kubwa)
- Kunywa maji ya kutosha. Angalau glasi nane kwa siku
- Kukojoa mkojo kabla na baada ya kujamiiana. Hii husaidia kuondoa wadudu katika njia ya mkojo
- Epuka kusafisha uke kwa kutumia sabuni kali zitakazoua hadi wadudu wanaosaidia kinga ya mwili
- Tumia pedi safi mara kwa mara na badilisha kila baada ya muda mfupi
- Osha sehemu za siri kwa maji ya moto au vuguvugu kabla ya kujamiiana
- Vaa nguo za ndani za pamba zinazoweza kupitisha hewa ya kutosha
- Ukiweza oga katika maji yanayotiririka kutoka bombani (bomba la mvua) na epuka kunawa maji yaliyokaa chooni au bafuni kwa muda mrefu
- Epuka kuvaa nguo za ndani zinazobana
MAMBO YA KUZINGATIA
Ugonjwa huu hutibika haraka na kwa urahisi sana. Wahi kituo cha kutolea huduma za afya kwa ushauri na matibabu
Ugonjwa huu huenezwa kwa njia nyingi. Ni vyema kuwa makini na zote ili kuwa salama zaidi
Ni vyema kuwahi matibabu na kumaliza dawa vizuri ili kuzuia usugu na madhara ya baadae ya ugonjwa huu
Ugonjwa huu huwaathiri na watoto pia. Ni vyema na wao wakakingwa vizuri ili wasiupate, na kutibiwa haraka endapo wakiupata na wao
Dalili nyingi za ugonjwa huu hufanana na zile za malaria na magonjwa mengine. Ni vyema kupata vipimo na ushauri wa daktari na washauri wa afya

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni