Jumapili, 3 Julai 2016

      MAGONJWA SUGU NA JINSI YA KUZUIA USUGU WA MAGONJWA

UTANGULIZI
Umewahi kusikia kuhusu Malaria sugu? Maambukizi katika nia ya mkojo (U.T.I.) sugu? Homa ya matumbo (Typhoid) sugu? 
                            


Usugu wa ugonjwa ni ile hali ya vijidudu vinavyosababisha ugonjwa kutokufa vyote kwa dawa au matibabu na hivyo kufanya ugonjwa kutopona kabisa. Matokeo yake ni vijidudu au ugonjwa kuendelea kuwepo mwilini hata kama mtu atatumia dawa vizuri kabisa. Tatizo la usugu linaweza likajitokeza kwa magonjwa mbalimbali yanasosababishwa na bakteria, protozoa, virusi nk kama vile Malaria, Maambukizi katika njia ya mkojo (U.T.I.), Kifua kikuu, Kansa, Ukimwi, Kisonono, Kaswende na mengineyo mengi.
Usugu huo hupelekea dawa za kawaida ambazo ndizo hutumika kuutibu ugonjwa kushindwa kutibu ugonjwa huo na kuhitaji dawa nyingine mpya au ya juu zaidi.
Tatizo la usugu wa magonjwa hupelekea kupungua kwa ufanisi wa dawa na hata dawa kukosa kabisa thamani ambayo ilikuwa nayo zamani.

UKUBWA WA TATIZO LA USUGU WA MAGONJWA


Tatizo la usugu wa magonjwa ni kubwa sana. Ni kubwa kiasi cha kufanya dawa nyingi ambazo zilikuwa zikitumika sana zamani kuanza kuachwa na kuondolewa kabisa katika matumizi. Unazikumbuka dawa za zamani kama vile Chloroquine na Tetracycline? Unaziona sana siku hizi?
Dawa zilizokumbwa zaidi na tatizo hili ni dawa za kutibu magonjwa ya bakteria, malaria, kansa na ukimwi.
Pia tatizo hili linaendelea kukua siku hadi siku. Matokeo yake ni kufeli kwa matibabu, kuongezeka kwa magonjwa, vifo na gharama kubwa za matibabu.
Mbaya zaidi ni kwamba usugu wa magonjwa huweza kuambukizwa kutoka kwa mgonjwa mmoja kwenda kwa mtu mwingine, na kumpelekea mtu huyo kuwa ugonjwa sugu. Na pia vijidudu vya magonjwa vinaweza kuwa na usugu kwa dawa nyingi au zote za kundi fulani la dawa.
Endapo ushirikiano na juhudi kubwa kulikabili tatizo hili hazitachukuliwa basi litakuwa kubwa zaidi na kuleta matatizo mengi na makubwa zaidi.
Kushirikiana ili kuzuia na kutokomeza tatizo hili ni jukumu letu sote; Wagonjwa, Watoa huduma za afya wote, Serikali na jamii nzima kwa ujumla.

SABABU ZA MAGONJWA KUWA SUGU
Usugu wa magonjwa hutokea pale vijidudu vya magonjwa vinapojijengea uwezo wa kupambana na dawa na kuweza kuepuka kuuwawa na dawa hiyo. Matokeo yake ni kwamba vijidudu hivyo kuendelea kuishi hata kama mtu atatumia dawa hiyo vizuri, na hivyo ugonjwa huo hautapona moja kwa moja kwa dawa hiyo.
Vitu vinavyosababisha au kusaidia usugu wa magonjwa ni pamoja na
1.      Kutofanya vipimo sahihi na kupata uhakika wa vijidudu vilivyosababisha ugonjwa na dawa ambayo itawaua vizuri kabisa
2.      Kutotumia dawa sahihi zaidi kwa vijidudu au ugonjwa husika
3.      Mgonjwa kutotumia dawa vizuri. Hii ni pamoja na kutomeza dawa kwa wakati, kutomeza dozi zote katika siku na kutomaliza dozi na dawa zote
4.      Muingiliano wa dawa na dawa zingine, magonjwa na hata vyakula hivyo kupunguza ufanisi wa dawa na kuviwezesha vijidudu vya magonjwa kutokufa na kuwa sugu
5.      Kuambukizwa vijidudu sugu kutoka kwa mgonjwa mwingine

MADHARA YA USUGU WA MAGONJWA
Usugu wa magonjwa na kushindwa kwa dawa kuua vijidudu vya magonjwa na kutibu magonjwa kuna hasara kubwa sana kiuchumi na kiafya. Madhara ya usugu wa magonjwa ni pamoja na
1.      Kufeli kwa matibabu na kuendelea kwa magonjwa, maumivu, homa na matatizo mengine ya kiafya
2.      Kuenea zaidi kwa magonjwa na kuongezeka kwa mzigo wa magonjwa katika jamii
3.      Kuongezeka kwa idadi vifo
4.      Wagonjwa kutumia muda mwingi zaidi kutibiwa na/au kulazwa hospitali
5.      Kuongezeka kwa gharama za matibabu kutokana na kutakiwa kutumia dawa zenye uwezo wa juu zaidi na hivyo kugharimu gharama kubwa zaidi

6.      Hasara katika kampuni na viwanda vya kuzalisha na kuuza dawa kutokana na kushindwa kuendelea kuuza vizuri dawa zao

                           
             



Madhara ya usugu wa magonjwa yanamuhusu kila mtu katika jamii. Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anachukua hatua ili kuzuia na kulitokomeza kabisa tatizo hili.

JINSI YA KUZUIA NA KUTOKOMEZA TATIZO LA USUGU WA MAGONJWA
Mpaka sasa nina imani umelielewa tatizo la usugu wa magonjwa na magonjwa sugu. Pia nina imani utakuwa tayari kukabiliana nalo ili kulizuia na kulitokomeza kabisa.
Tunaweza kulizuia na kulitokomeza kabisa tatizo hili kwa
1.      Kufanya vipimo sahihi na kupata uhakika wa vijidudu vilivyosababisha ugonjwa na dawa ambayo itawaua vizuri kabisa
    


2.      Kutumia dawa sahihi zaidi kwa vijidudu au ugonjwa husika. Na hili hujulikana baada ya kufanya vipimo na majaribio ya maabara
3.      Kutumia dawa vizuri. Hii ni pamoja na kumeza dawa kwa wakati, kumeza dozi sahihi, kumeza dozi zote katika siku na kumaliza dozi na dawa zote.
Tumia dawa zote kama ulivyoelekezwa na daktari, mfamasia, nesi na kadhalika
4.      Wataalam wa dawa kushirikiana na madaktari ili kutoa dawa bila kuwa na muingiliano wa dawa na dawa zingine, magonjwa na hata vyakula.
Pia wakati wa matibabu na kupewa dawa mgonjwa aeleze kama ana magonjwa mengine na kuna dawa zingine anazitumia
5.      Kujikinga ili kutoambukizwa vijidudu vya magonjwa kutoka kwa wagonjwa wengine
Hapa ni suala la kuzingatia kanuni zote za afya za kuzuia magonjwa na kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali 
6.      Kutoa elimu kwa umma na kushirikiana juu ya tatizo la usugu wa magonjwa na jinsi ya kulitokomeza


Tatizo la usugu wa magonjwa na kufeli kwa dawa ni kubwa lakini linaweza kutokomezwa kabisa. Jamii nzima tushirikiane ili kutokomeza tatizo hili na tuwe na afya bora.


Jumatano, 29 Juni 2016

       MAAMBUKIZI KATIKA NJIA YA MKOJO (U.T.I)
Maambukizi katika njia ya mkojo ni ugonjwa au maambukizi yanayotokea kwenye njia ya mkojo na kusababisha maumivu, homa, kukosa nguvu, harufu mbaya ya mkojo na maumivu wakati wa kukojoa. Husababishwa na bakteria ambao wanaingia kwenye mwili kupitia kwenye uke au uume wakati wa kujamiiana, kuwekewa mpira wa kukojolea, wakati wa kutawadha au ukuaji wa bakteria wakati wa uvaaji pedi na nguo za ndani.
Maambukizi haya huweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kupitia kujamiiana, na pia mtu anaweza kuyapata bila hata kujamiiana kama ilivyooneshwa hapo juu.
Huweza kumpata mtu yeyote, lakini watu walio katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi haya ni wanawake, na zaidi ni wanawake wajawazito. Pia wazee, wagonjwa wa tezi dume, wagonjwa waliowekewa mipira ya kukojolea, wagonjwa wa kisukari na wagonjwa wenye upungufu wa kinga ya mwili.
JINSI MAAMBUKIZI YA NJIA YA MKOJO (U.T.I.) YANAVYOTOKEA NA KUENEZWA
Maambukizi ya njia ya mkojo huwapata watu kupitia njia zifuatazo
- Kujamiiana na mtu mwenye maambukizi bila kutumia kinga
- Kueneza bakteria kutoka kwenye kinyesi (njia ya haja kubwa) kwenda kwenye uke (njia ya mkojo) wakati wa kujitawadha kwa kunawa kutokea nyuma (kwenye njia ya haja kubwa) kuja mbele (kwenye njia ya haja ndogo)
- Kukua kwa bakteria kupitia mipira ya kukojolea wagonjwa, pedi na nguo za ndani
- Kutawadha maji yenye bakteria wanaoweza kusababisha maambukizi katika njia ya mkojo
- Kukua kwa bakteria kupita kiasi katika njia ya mkojo kutokana na kupungua kwa kinga ya mwili
DALILI ZA MAAMBUKIZI KATIKA NJIA YA MKOJO (UTI) Maambukizi katika njia ya mkojo huwa na dalili zifuatazo
- Maumivu wakati wa kukojoa na kuhisi kama unaungua kwa ndani ya njia ya mkojo
- Kujisikia kukojoa mara kwa mara, ila kupata mkojo kidogo tu
- Maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo
- Homa
- Uchovu na kupungukiwa na nguvu
- Rangi ya mkojo kubadilika na kuwa kama nyekundu au pinki (japo kwa mbali)
- Mkojo kuwa na uchafu kama 
- Kichefuchefu na kutapika

MADHARA YA BAADAE YA MAAMBUKIZI KATIKA NJIA YA MKOJO (U.T.I)Mara nyingi ugonjwa huu hudhibitiwa vizuri na dawa na hakuna madhara makubwa yatakayojitokeza. Vinginevyo kama ukichelewa kutibiwa unaweza kupata uharibifu wa Ini. Matokeo yake ni kujifungua kabla ya miezi tisa na kuzaa watoto wenye uzito mdogo. Ni vyema kupata matibabu mazuri na kwa wakati ili kuweza kuzuia uharibifu na matatizo mengine yoyote yanayoweza kujitokeza baadae.
MATIBABU YAKE
Kuna dawa nyingi sana za kutibu ugonjwa huu wa maambukizi katika njia ya mkojo. Cha msingi ni kufanya vipimo na kujua bakteria au wadudu wengine waliosababisha ugonjwa na kujua dawa nzuri zaidi kwa ajili ya kuwaua. Unashauriwa kumuona daktari na kupata matibabu sahihi ili kuweza kupona kabisa ugonjwa huu.
Zipo dawa nyingi kwa ajili ya ugonjwa huu. Baadhi yao huweza kutumika kwa mtu yeyote (Mifano Amoxicillin na Ampicillin) na nyingine haziwezi kutumika kwa baadhi ya watu kama vile Doxycycline haiwezi kutumika kwa watoto na Tetracycline haiwezi kutumika kwa akina mama wajawazito.


Usitumie dawa yoyote bila kushauriwa na daktari. Na hakikisha unatumia dawa zote kama ulivyoelekezwa na daktari na mfamasia, ikiwa ni pamoja na kumaliza dozi hata kama utajihisi umepona kabla ya kumaliza dawa.












JINSI YA KUJIKINGA DHIDI YA MAAMBUKIZI YA NJIA YA MKOJO (U.T.I.)Uzuri wa maambukizi haya ni kwamba huweza kuepukwa au kuzuiliwa kabisa. Mtu anaweza kujikinga kwa
- Kuepuka kujamiiana bila kutumia kinga
- Kunawa vizuri wakati wa kujitawadha kwa kuanzia mbele (njia ya haja ndogo) kwenda nyuma (njia ya haja kubwa)
- Kunywa maji ya kutosha. Angalau glasi nane kwa siku
- Kukojoa mkojo kabla na baada ya kujamiiana. Hii husaidia kuondoa wadudu katika njia ya mkojo
- Epuka kusafisha uke kwa kutumia sabuni kali zitakazoua hadi wadudu wanaosaidia kinga ya mwili
- Tumia pedi safi mara kwa mara na badilisha kila baada ya muda mfupi
- Osha sehemu za siri kwa maji ya moto au vuguvugu kabla ya kujamiiana
- Vaa nguo za ndani za pamba zinazoweza kupitisha hewa ya kutosha
- Ukiweza oga katika maji yanayotiririka kutoka bombani (bomba la mvua) na epuka kunawa maji yaliyokaa chooni au bafuni kwa muda mrefu
- Epuka kuvaa nguo za ndani zinazobana
MAMBO YA KUZINGATIA
Ugonjwa huu hutibika haraka na kwa urahisi sana. Wahi kituo cha kutolea huduma za afya kwa ushauri na matibabu
Ugonjwa huu huenezwa kwa njia nyingi. Ni vyema kuwa makini na zote ili kuwa salama zaidi
Ni vyema kuwahi matibabu na kumaliza dawa vizuri ili kuzuia usugu na madhara ya baadae ya ugonjwa huu
Ugonjwa huu huwaathiri na watoto pia. Ni vyema na wao wakakingwa vizuri ili wasiupate, na kutibiwa haraka endapo wakiupata na wao
Dalili nyingi za ugonjwa huu hufanana na zile za malaria na magonjwa mengine. Ni vyema kupata vipimo na ushauri wa daktari na washauri wa afya

Alhamisi, 23 Juni 2016

MAMBO (YA KITABIA) YANAYOKUWEKA KATIKA HATARI YA KUPATA KISUKARI

Ugonjwa wa kisukari huweza kusababishwa au kuchangiwa na mambo mbalimbali ya ndani na nje ya mwili. Mengine tuna uwezo wa kuyaratibu na kurekebisha sisi wenyewe tena kwa urahisi tu.

Miongoni mwa mambo hayo ni
1. Kukosa mazoezi au kufanya mazoezi kidogo sana
2. Uvutaji wa sigara













3. Msongo
4. Kulala sana au kutolala vya kutosha
Kwa bahati nzuri hayo mambo yote ni ya kitabia na unaweza kuyarekebisha. Unaweza ukajilinda dhidi ya kisukari kwa
i. Kupunguza uzito na mwili wenye afya nzuri
ii. Kujishughulisha kwa mambo mbalimbali kama vile kazi zinazotumia nguvu, misuli na mazoezi 
iii. Kula vizuri
Epuka kula kwa wingi vyakula vya wanga, sukari, mafuta na nyama nyekundu na za kupakiwa kiwandani
iv. Acha kuvuta sigara
Ukizingatia hayo utakuwa umejiepusha kupata kisukari au itakusaidia sana kuwa na afya nzuri hata kama una kisukari

Jumatatu, 13 Juni 2016

MAKOVU YA CHUNUSI

MAKOVU YA CHUNUSI
Kwa ushauri zaidi wasiliana nasi kwa :
0 659 528 724 au 0 784 082 847

Makovu ya chunusi ni matokeo ya kupona kwa vidonda au majeraha yaliyosababishwa na kupasuliwa kwa chunusi. Makovu hayo huweza kuwa mengi au machache, makubwa au madogo, yaliyoanzishwa ndani zaidi au yaliyo juu juu na kadhalika. Yote kwa yote Makovu hayo yanaweza kupunguzwa au kuondolewa kabisa.
JINSI YA KUZUIA MAKOVU YA CHUNUSI
Njia nzuri kabisa ya kuzuia Makovu ni kutopasua chunusi. Yaani tumia dawa au vipodozi hadi chunusi zipone zenyewe salama salmin, lakini usipasue hata moja! Ni rahisi zaidi kuondoa chunusi kuliko Makovu yake.
JINSI YA KUYAPUNGUZA AU KUONDOA MAKOVU YA CHUNUSI
Makovu ya chunusi huweza kupunguzwa au kuondolewa kwa kuondoa seli za ngozi zilizokufa na kuwa kovu. Hili huweza kufanywa kwa kutumia dawa au vipodozi vyenye uwezo wa kuondoa sehemu ya nje ya ngozi ambayo ndiyo haswa hukaliwa na Makovu hayo.
Mfano wa kipodozi hapa ni Scrub; lakini ni lazima Scrub hiyo iwe sahihi kwa ngozi ya mtu husika na itumike vizuri.
Kwa upande wa dawa utapata ushauri wa daktari (Kwa kuwa dawa haziruhusiwi kuandikwa hapa nakushauri pata ushauri wa daktari/mtaalam wa afya)
USHAURI
Kwanza unashauriwa usitumie vipodozi vikali na visivyo salama kuondoa Makovu. Vipodozi hivyo vitaharibu ngozi yako na kuhatarisha afya yako mara dufu
Pili unashauriwa kutojichubua wala kutumia njia nyingine yoyote isiyofaa. Hizo zitakuharibia afya yako na pia baada ya muda Makovu yatarudi pale pale
Tatu unashauriwa kutumia vipodozi au dawa kama ulivyoelekezwa na mtaalam wa Afya. Kama ni kwa wiki mara mbili basi usizidishe mara mbili, kama baada ya kupaka usitembee juani basi usitembee juani baada ya kupaka.
Tatu unashauriwa kula mlo kamili na kupumzika vya kutosha ili kuisaidia ngozi yako kujijenga vizuri na kubadilisha sehemu zenye Makovu kuwa ngozi mpya isiyo na makovu
Uzuri wa Makovu ya chunusi ni kwamba yanatibika na kuweza kuondolewa kabisa. Tena hata ndani ya muda mfupi. Cha msingi ni kupata ushauri mzuri kutoka kwa wataalam na kutumia bidhaa (vipodozi au dawa) nzuri na kutumia vizuri.
S&E BEAUTY SOLUTIONS inakukaribisha na inakutakia kila la heri katika mchakato wa kuzuia na kuondoa Makovu ya chunusi.

MATUMIZI YA NETI TU HAYATOSHI KUZUIA MALARIA

MATUMIZI YA NETI TU HAYATOSHI KUZUIA MALARIA
Ushawahi kujiuliza ni kwa nini unaweza ukawa unalala kwenye neti kila siku lakini bado ukapata malaria? 
Na kuna watu wengi ambao wamepata malaria hali ya kuwa wanalala ndani ya chandarua kila siku? 
Sababu ni rahisi sana. KUNG'ATWA NA MBU UKIWA NJE YA NETI. HUSUSAN KABLA YA KULALA KITANDANI
Muda wa kuanzia saa 12 jioni mpaka saa 4 usiku watu wengi hung'atwa na mbu na kuweza kupata malaria. Huu ndo ule wakati wa maongezi ya jioni nje, ukumbini au chumbani; kuangalia televisheni sebuleni, kuwa karibu na bustani ukipata chakula na vinywaji, umepumzika sebuleni au chumbani na kadhalika. Mara nyingi tunakuwa nje ya chandarua muda huo na huweza KUNG'ATWA na mbu.
JINSI YA KUJIKINGA
Wakati upo nje ya neti jikinge dhidi ya kung'atwa na mbu kwa kufanya yafuatayo :
1. Vaa nguo zinazofunika mwili wako wote





Hapa unashauriwa kuvaa suruali na mashati ya mikono mirefu, gauni refu na lenye mikono mirefu, soksi zisizoweza kupenyezwa na mdomo wa mbu nk
2. Paka dawa ya kuzuia mbu wasikung'ate wala kutua mwilini mwako
Kwa Kiingereza ndizo huitwa "mosquito repellents". Hizi husaidia kufukuza na kuwazuia mbu wasikung'ate kabisa

3. Tumia dawa za kuzuia malaria
Hususan kama unatoka sehemu ambayo haina malaria kwa wingi kwenda sehemu yenye tatizo kubwa la malaria. Pata ushauri wa daktari ili kufanikisha jili
4. Hakikisha usafi wa mazingira na kutokomeza mazalia ya mbu
Haya hujumuisha madimbwi ya maji, vichaka nk



5. Epuka maeneo yenye mbu muda wa jioni
Inawezekana ukawa upo mbali na nyumbani au ukashindwa kufanya mambo ya hapo juu. Hapa cha msingi jiepushe na maeneo yenye mbu, kama vile yaliyo na giza na yaliyopo karibu na mazalia ya mbu.
MALARIA INAZUILIKA. TUANZE SASA.......





MAFUTA NA LOSHENI SAHIHI KWA NGOZI YAKO

MAFUTA NA LOSHENI SAHIHI KWA NGOZI YAKO
Kama mnavyojua ngozi zetu zinatofautiana. Kuna watu wenye ngozi kavu, kuna wenye ngozi za mafuta, kuna wenye ngozi za kawaida (sio kavu wala sio za mafuta) na wenye ngozi mchanganyiko.
Kwa upande wa mafuta na losheni pia kuna mafuta na losheni kwa ajili ya ngozi kavu, kuna ya ngozi za kawaida, kuna ya ngozi mchanganyiko na ya ngozi za mafuta.
Bahati mbaya ni kwamba vipodozi vingi vinatoka nje, na vimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza. Sasa cha msingi ni kujua aina ya ngozi yako kwanza na kisha kuchagua mafuta na losheni inayofaa kwa ngozi yako.
Pima ngozi yako sasa. Unaweza kufanya hivi hospitali, maduka ya urembo na Vipodozi nk
Pia S&E HEALTH SOLUTIONS vipimo vyake vinapatikana na unaweza kutumiwa popote Tanzania.
Baada ya kujua aina ya ngozi yako sasa nunua na tumia mafuta au losheni inayoendana nayo.
1. Kama ngozi yako ni kavu tumia losheni iliyoandikwa FOR DRY SKIN
2. Kama ngozi yako ni ya mafuta tumia losheni iliyoandikwa FOR OILY SKIN
3. Kama ngozi yako ni ya kawaida tumia losheni iliyoandikwa FOR NORMAL SKIN
4. Kama ngozi yako ni mchanganyiko tumia losheni iliyoandikwa FOR COMBINATION SKIN

Pia kuna mafuta na losheni ambayo yanafaa kwa aina zote za ngozi. Haya huweza kutumiwa na mtu mwenye ngozi ya aina yoyote. Yenyewe utakuta imeandikwa FOR ALL SKIN TYPES.

Mafuta na losheni zinazoendana na aina ya ngozi yako ndiyo vitakupa matokeo mazuri bila kuathiri ngozi yako kama vile kukuletea chunusi, jasho jingi nk
S&E HEALTH SOLUTIONS inakutakia kila la kheri katika kuboresha afya na uzuri wako!


VIPODOZI VISIVYO SALAMA NA MADHARA YAKE
SEMINA HII IMEANDALIWA NA KULETWA KWAKO NA:
S&E HEALTH SOLUTIONS
WATAALAM NA WASHAURI WA AFYA, UREMBO NA VIPODOZI
ILALA BUNGONI, DAR ES SALAAM
0 659 528 724 , 0 784 082 847

SEHEMU YA PILI

2.0 MADHARA YA VIPODOZI VISIVYO SALAMA
Vipodozi visivyo salama vina madhara mengi sana kwa afya ya mtumiaji. Na kama mtumiaji ni mjamzito basi madhara hayo yanaweza kumpata na mtoto aliyepo tumboni.
Pia vipodozi hivi vina athari nyingi sana kiuchumi kwani vitapelekea mtu kutumia pesa tena kugharamia matibabu ya matatizo atakayopata.
Madhara hayo ni pamoja na:
-Ugonjwa wa saratani (kansa) ya ngozi, maini, ubongo, mapafu, mfumo wa damu, utumbo mpana na kibofu cha mkojo
-Uharibifu wa ngozi, macho, ini, mapafu na figo
-Magonjwa ya moyo na kutopumua vizuri
-Kutokwa na chunusi kubwa kubwa
-Ngozi kuungua, maumivu makali, ngozi kuwa nyekundu na kutokwa na vipele
-Ngozi kuwa nyembamba sana na laini na endapo ngozi itapata jeraha au kufanyiwa upasuaji, kidonda kitachelewa kupona au hakitapona
-Mzio (Allergy) na muwasho wa ngozi
-Kichefuchefu, kutapika, kusikia usingizi na kizunguzungu
-Magonjwa ya akili, mishipa ya fahamu (hasa kichwani)
-Uharibifu wa ubongo na mtindio wa ubongo kwa watoto wachanga na waliopo tumboni
-Ngozi kuwa laini na kusababisha kupata magonjwa kama fangasi kwenye ngozi au maambukizi ya vimelea vya maradhi
-Kuchubuka kwa ngozi
-Ngozi kuwa na mabaka meusi na meupe au rangi mbalimbali
-Upofu, uziwi na upotevu wa fahamu wa mara kwa mara
-Kuumwa kichwa, kusikia kizunguzungu na kupoteza fahamu
2.2 USHAURI
Kama tulivyoona hapo juu mengi ya madhara ya vipodozi visivyo salama ni makubwa na huhatarisha kabisa afya za watumiaji na watoto. Hivyo ni vyema kuvijua na kuviepuka kabisa ili usiweze kupata madhara.
Pili msaidie kumuelimisha ndugu, jamaa na rafiki na yeye ajue na asitumie kabisa vipodozi visivyo salama
Pia ukiona mtu au duka ambalo linauza vipodozi visivyo salama acha kununua vipodozi kutoka kwake na toa taarifa kwa mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa
Epuka kabisa vipodozi visivyo salama. Hata kama vinakuletea matokeo mazuri kiasi gani.